Jumatatu ya 29 Mwaka
· Mwaka C
Somo la Kwanza
Efe. 2:1 – 10Ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya Imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
Neno la Bwana. — Tumshukuru Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab. 100Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake.
Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.
K. Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake.
Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
K. Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake.
Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake.
K. Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake.
Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
K. Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake.
Shangilio la Injili
Yn. 8:12Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.
Injili
Lk. 12;13-21Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.
Injili ya Bwana. — Sifa kwako, Ee Kristo.
Maoni (0)
Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kutoa maoni.
Ingia utoe maoni