Jumatano. 04 Februari. 2026

Mt. Maria Goretti

Maria Goretti

Maria Goretti alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1890 katika kijiji kidogo huko Corinaldo, Italia. Familia yake ilikuwa maskini sana, lakini ilijulikana kwa imani na mshikamano wa kifamilia. Maria alikuwa mtoto wa pili kati ya watoto sita.

Baba yake, Luigi, alifariki akiwa mdogo, na familia ikalazimika kuhamia mji mwingine kutafuta kazi. Walipanga katika nyumba ndogo ya kukodisha pamoja na familia nyingine; familia ya Serenelli.

Na hapa ndipo historia yake ilipoanza kubadilika.

"Marietta" alikuwa binti mwenye upendo, alikuwa msichana mpole, mnyenyekevu, na mcha Mungu. Ingawa hakufanikiwa kwenda shule kwa sababu ya kazi nyingi za nyumbani; alijua kusali, na kila siku alisali rozari.

Hakuwa na nguo nyingi wala viatu vizuri, lakini moyo wake ulikuwa na upendo na heshima kwa kila mtu. Wengi walimpenda kwa tabasamu lake na heshima yake.
Miongoni mwa familia ya Serenelli; kulikuwa na kijana aitwaye Alessandro Serenelli, mwenye umri wa miaka 20. Siku zilikwenda na kijana alianza kumtamani Maria, alimtamani kingono. Siku moja alimwendea, na mara kadhaa alimwendea tena na tena akijaribu kumbembeleza afanye naye zinaa, lakini Maria alikataa kila mara, akisema:
“Hapana, Alessandro! Hii ni dhambi, na Mungu hataki!”
Ingawa jambo hilo lilimkosesha raha Maria ila hakumwambia mtu, kwa kuwa alikuwa anaogopa kuleta ugomvi kati ya familia hizo mbili.

Tarehe 5 Julai 1902, mama yake Maria alikuwa shambani na watoto wengine, akimuacha Maria nyumbani akishona nguo. Alessandro aliona huo ni wakati mujarab hivyo alimfuata tena nyumbani na kumkuta peke yake. Alijaribu kumshika na kumvuta, akajaribu kumlazimisha kumfanyia kitendo. Maria alipiga kelele na kupinga kelele kwa nguvu.

Alipoona hatokubali, Alessandro alijawa na hasira alichukua kisu cha jikoni na kumchoma mara kadhaa (takriban mara 14). Maria alianguka chini, akilia kwa uchungu.

Alessandro, akiwa na hasira na aibu, alitoroka na kutokomea. Maria alipelekwa hospitali haraka.

Hospitalini, madaktari walijaribu kumwokoa, lakini majeraha yalikuwa mabaya sana. Wakati wa mateso yake, Maria alisema wazi kwa wazazi wake kwamba amemsamehe Alessandro.

Siku iliyofuata, 6 Julai 1902, Maria alifariki akiwa na umri wa miaka 11 tu.

Alessandro alikamatwa na kufungwa miaka 30. Mwanzo alikataa kujutia kosa lake, lakini miaka mingi baadaye, akiwa gerezani, alianza kuota ndoto ambapo Maria alimtokea akimletea maua meupe kama ishara ya usafi na msamaha. Ndipo moyo wake ulipobadilika.

Alipotoka gerezani, jambo la kwanza alilofanya ni kwenda kumwomba msamaha mama wa Maria, ambaye alimkumbatia na kusema; “Maria alikusamehe, na nami nakusamehe.”

Baadaye, Alessandro aliishi maisha ya imani na utulivu, alifanyia kazi bustani ya kanisa hadi kifo chake.

Mnamo mwaka 1950, Papa Pius XII alimtangaza Maria Goretti kuwa Mtakatifu mbele ya hadhira kubwa, ikiwemo mama yake mwenye umri wa miaka 82.
Maria alitangazwa kuwa mlezi wa vijana, wasichana, na usafi.

Maoni


Ingia utoe maoni