Jumatano ya 5 ya Mwaka
· Mwaka B · Juma la 1 la Zaburi
Somo la Kwanza
1Fal. 10:1-10Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hakima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa naye, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amkufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.
Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.
Neno la Bwana. — Tumshukuru Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab. 37:5-6, 30-31, 39-40Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Umkabidhi Bwana njia yako,
Pia umtumaini naye atafanya.
Akaitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri.
K. Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Kinywa cha mwenye haki hunena hekima,
Na ulimi wake husema hukumu.
Sheria ya Mungu wake imo moyoni mwake,
Hatua zake hazitelezi.
K. Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Wokovu wa wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
Huwaopoa wasio haki na kuwaokoa,
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
K. Kinywa cha mwenye haki hunena hekima.
Shangilio la Injili
Yn. 17:17Ee Bwana, neno lako ndiyo kweli, uwatakase kwa hiyo kweli.
Aleluya.
Injili
Mk. 7:14 – 23Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.
Injili ya Bwana. — Sifa kwako, Ee Kristo.
Maoni (0)
Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kutoa maoni.
Ingia utoe maoni