Ijumaa ya 14 ya Mwaka
· Mwaka A · Juma la 2 la Zaburi
Somo la Kwanza
Mwa. 46 :1-7, 28-30Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri.
Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake, kitambo kizima. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai.
Neno la Bwana. — Tumshukuru Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab. 37 :3-4, 18-19, 27-28, 39-40Wokovu wa wenye haki una Bwana.
Umtumaini Bwana ukatende mema,
ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
naye atakupa haja za moyo wako.
K. Wokovu wa wenye haki una Bwana.
Bwana anazijua siku za wakamilifu,
na urithi wao utakuwa wa milele.
Hawataaibika wakati wa ubaya,
na siku za njaa watashiba.
K. Wokovu wa wenye haki una Bwana.
Jiepue na uovu, utende mema,
na kukaa hata milele.
Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
wala hawaachi watauwa wake.
K. Wokovu wa wenye haki una Bwana.
Na wokovu wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa,
kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
K. Wokovu wa wenye haki una Bwana.
Shangilio la Injili
Yak. 1 :21Pokeeni kwa upole neno la Mungu
lililopandwa ndani,
liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.
Injili
Mt. 10 :16-23Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.
Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.
Injili ya Bwana. — Sifa kwako, Ee Kristo.
Maoni (0)
Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kutoa maoni.
Ingia utoe maoni