Jumanne ya 5 ya Mwaka
· Mwaka A
Somo la Kwanza
Mwa. 1:20 – 2:4Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufungwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufungwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitaambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.
Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu; kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.
Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wan chi yote, pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wan chi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.
Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.
Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa.
Neno la Bwana. — Tumshukuru Mungu.
Wimbo wa Katikati
Zab. 8:3 – 8Wewe Mungu, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote.
Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
Mwezi na nyota ulizoziratibisha;
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie?
K. Wewe Mungu, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote.
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
K. Wewe Mungu, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote.
Kondoo, na ng’ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni;
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitiacho njia za baharini.
K. Wewe Mungu, Bwana wetu, jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote.
Shangilio la Injili
Zab. 27:11Ee Bwana, unifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.
Injili
Mk. 7:1-13Basi wale Mafarisayo na waandishi wakamwuliza, Mbona wanafunzi wako hawaendi kwa kuyafuata mapokeo ya wazee, bali hula chakula kwa mikono najisi? Akawambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami; Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu.
Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema? Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu. Maana Musa alisema, Waheshimu baba yako na mama yako, na, amtukanaye babaye au mamaye kufa na afe. Bali ninyi husema, Mtu akimwambia babaye au mamaye. Ni Korbani, yaani, wakfu, kitu changu chochote kikupasacho kufaidiwa nacho, huwa basi; wala hammruhusu baada ya hayo kumtendea neno babaye au mamaye; huku mkilitangua neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyopokeana; tena mwafanya mambo mengi yaliyo sawasawa na hayo.
Injili ya Bwana. — Sifa kwako, Ee Kristo.
Maoni (0)
Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kutoa maoni.
Ingia utoe maoni