Ruka hadi maudhui
Mkatoliki Leo
← Masomo yote Kwaresima · Rangi ya Zambarau

Dominika ya 2 ya Kwaresima

· Mwaka A · Juma la 2 la Zaburi

Somo la Kwanza

Mwa 12:1-4a
Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru;

Neno la Bwana. — Tumshukuru Mungu.

Wimbo wa Katikati

Zab 33:4-5, 18-20, 22
K.

Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.

K. Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa.

K. Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe.

K. Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Somo la Pili

2 Tim 1:8b-10
Uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili;

Neno la Bwana. — Tumshukuru Mungu.

Shangilio la Injili

Mt 17:5
Sauti ya Baba ilitoka katika wingu jeupe: "Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye."

Injili

Mt 17:1-9
Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana. Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope. Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.

Injili ya Bwana. — Sifa kwako, Ee Kristo.

0 Maoni
Tafakari ya masomo haya Kwaresima: Muda wa Kumfahamu Yesu! →

Maoni (0)

Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kutoa maoni.

Ingia utoe maoni