Ruka hadi maudhui
Mkatoliki Leo
← Masomo yote Kipindi cha Kawaida · Rangi ya Kijani

Ijumaa ya 32 ya Mwaka

· Mwaka B · Juma la 4 la Zaburi

Somo la Kwanza

2Yoh. 1:4 – 9
Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba. Na sasa, mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane.
Na huu ndio upendo; tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.

Neno la Bwana. — Tumshukuru Mungu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 119:1 – 2, 10 – 11, 17 – 18
K.

Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.

K. Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi.

K. Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
Unifumbue macho yangu niyatazame
Maajabu yatokayo katika sheria yako.

K. Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Shangilio la Injili

Zab. 119:28, 33
Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya.

Injili

Lk. 17:26-37
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulikunya moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu yeyote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na yeyote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia. Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.

Injili ya Bwana. — Sifa kwako, Ee Kristo.

0 Maoni
Tafakari ya masomo haya Kujiweka Tayari kwa Upendo →

Maoni (0)

Bado hakuna maoni. Kuwa wa kwanza kutoa maoni.

Ingia utoe maoni