Masomo ya Misa
Jumamosi ya 9 ya Mwaka (Jumamosi, Juni 06, 2026)
2 Tim 4:1-8
Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti; nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako. Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.
Zab 71:8-9, 14-17, 22
Kinywa changu kitajazwa sifa zako, Na heshima yako mchana kutwa.
Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Nami nitatumaini daima, Nitazidi kuongeza sifa zake zote.
Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa;
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU; Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Nami nitakushukuru kwa kinanda, Na kweli yako, Ee Mungu wangu.
Nitakuimbia Wewe kwa kinubi, Ee Mtakatifu wa Israeli.
(K)Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa.
Mt 5:3
Aleluya, aleluya
Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Aleluya
Mk 12:38-44
Yesu aliwaambia katika mafundisho yake: Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa. Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.

Maoni
Ingia utoe maoni